MFUMUKO WA BEI YA MAFUTA: Namna vita ya Urusi na Ukraine inavyochangia kupanda kwa bei ya mafuta na hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na mfumuko huo nchini Tanzania.
Moja kati ya mijadala mizito iliyozuka mitandaoni katika siku za hivi karibuni ni suala la kupanda kwa bei ya mafuta hadi kufikiwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kuwepo katika soko la dunia kwa takribani miaka 14 sasa. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Mei 3 mwaka huu ilitangaza bei mpya kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kutumika kuanzia Mei 4 hapa nchini. Huku hali ya taharuki ikizuka kutokana na bei hizo kuwa juu sana mfano, bei elekezi ya mafuta ya petroli kwa rejareja jijini Dar-es-salaam ikiwa ni Tsh.3,148/= na bei ya dizeli ikiwa ni Tsh.3,264/=, serikali imekwisha toa tamko bungeni juu ya hatua za dharura zitakazochukuliwa. Aidha, watu wengi wamekuwa wakihoji uwiano na uhusiano wa kupanda kwa bei ya mafuta na sababu kubwa inayoelezwa kuwa ndiyo chanzo; vita ya Urusi na Ukraine.
Ni kwa
vipi vita ya Urusi na Ukraine inapelekea mfumuko wa bei ya mafuta?
Mnamo
Februari 24 mwaka huu, nchi ya Urusi iliivamia na kuingia ndani ya mipaka ya
nchi ya Ukraine katika kile ambacho rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin amekiita
‘operesheni maalumu’ baada ya vuguvugu ya muda mrefu na mzozo kati ya nchi hizo
mbili ulioanza tangu mwaka 2014. Aidha, mgogoro huu umezua athari za moja kwa
moja na zinginezo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuyumbisha sekta ya uchumi
kwa kusababisha mfumuko wa bei ya moja kati ya bidhaa muhimu zaidi duniani ya
mafuta. Kufuatia uvamizi wa Urusi kwenye mipaka ya Ukraine, jamii ya kimataifa
imechukua na inaendelea kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya Urusi ikiwemo
vikwazo vya kiuchumi (Economic Sanctions) ili kudhoofisha uchumi wake kwa
kuitenga na soko la dunia na kuinyima nchi hiyo namna za kupata mahitaji yake
muhimu ya uzalishaji ikiwemo teknolojia na uuzaji mafuta yake kwenda nchi
zingine kwa matumaini ya kuwa hatua hizi pengine zitaifanya Urusi kusalimu amri
na kusitisha mapigano dhidi ya Ukraine kwa kukosa vitendea kazi na rasilimali
za kuendeleza mapigano. Nchi za Umoja wa Ulaya kwa mfano, zilitangaza mipango
ya kuweka vikwazo hivyo ikiwemo katazo la kuingiza mafuta kutoka Urusi katika
nchi zilizo kwenye umoja huo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Kufikia
Jumatano, Mei 11, kiasi cha mafuta kutoka Urusi yaliyokuwa yakipitia Ukraine
kwenda Ulaya kilipungua kwa karibu robo nzima baada ya Kyiv kusimamisha
usafirishwaji kupitia mkondo ulioko nchini humo huku ikilaumu muingiliano
uliosababishwa na majeshi ya Urusi na kupelekea kufungwa kwa mkondo huo
uliokuwa ukisafirsha karibu asilimia nane ya mafuta kutoka Urusi kwenda Ulaya
kwa nchi kama Austria, Italy, Slovakia na nchi zingine zilizoko mashariki mwa
bara la Ulaya. Kampuni kubwa ya mafuta kutoka Urusi, Gazprom imesema kuwa
ufungwaji wa mkondo huu unahatarisha upatikanaji wa mafuta katika nchi za
ulaya.
Nchi ya
Urusi inashika nafasi ya pili duniani, nyuma ya Saudi Arabia katika uzalishaji
wa mafuta huku ikiuza karibu theluthi moja ya mafuta yapatikanayo Ulaya.
Kufuatia vikwazo vya kiuchumi vinavyowekwa dhidi yake, Urusi imejikuta katika
hali ngumu kwenye ufanyaji wa biashara kimataifa ikiwemo kutouza mafuta yake
katika baadhi ya nchi. Kutokana na utandawazi na dunia kuzidi kuunganika zaidi
na zaidi, athari za vita hii pamoja na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya urusi
zimesambaa duniani kote. Vikwazo hivi vimepelekea kupungua kwa kiasi cha mafuta
katika soko la dunia na hivyo kuwepo kwa uhaba ambao umesababisha bei kupanda
kufikia viwango vya juu zaidi kuliko vile vilivyoweka rekodi mwaka 2008.
Kufikia Machi 7, bei ya mafuta ya petroli ilipanda kwa senti 41 zaidi na
kuvunja rekodi ya $4 iliyofikiwa miaka 14 iliyopita nchini Marekani. Hata
hivyo, licha ya vita hii, tayari bei za mafuta zilikwishaanza kupanda kutokana
na kufunguka kwa shughuli za kiuchumi kutoka kwenye janga la corona. Watabiri
na wachambuzi wa masuala ya uchumi pia wamekuwa wakitabiri kuwepo kwa uhaba wa
mafuta kwa muda sasa na hivyo kupelekea manunuzi mengi ya ghafla kufanyika na nchi
mbalimbali (Speculative Oil Buying) kwa hofu ya uhaba huo kupelekea bei ambazo
hazitakuwa rafiki kabisa kwao au pengine kukosa kabisa mafuta. Hali hii pamoja
na msukumo kwa nchi zingine zinazozalisha mafuta kuzalisha mafuta zaidi kufidia
pengo linaloachwa sokoni na Urusi limepelekea kufumuka kwa bei ya bidhaa hii
muhimu hasa Mashariki ya Kati ambako nchi yetu Tanzania huagiza mafuta kwa
asilimia kubwa.
Jambo la
kufahamu ni kwamba kuna vitu vingi ambavyo husaidia kutathmini bei ya mwisho ya
mafuta kwa mtumiaji. Vitu hivyo ni kama bei ya mafuta katika soko la kimataifa,
gharama ya usafishaji wa mafuta (Oil refining costs), gharama ya utunzaji na
usafirishaji wa mafuta, ushuru wa serikali na faida kwa wauzaji wa jumla na
wale wa rejareja. Nchi ya Tanzania haina visima vya mafuta wala mitambo ya
kuchakata mafuta ghafi kama alivyosema Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba
bungeni wakati akiwasilisha kauli ya serikali kutokana na kupanda kwa bei ya
mafuta nchini. Hivyo, uhaba unaokuwepo duniani unatuathiri moja kwa moja na
kupelekea bei ya mafuta kupanda. Kutokana na kuagiza nje mafuta haya angalau
miezi miwili kuingia nchini. Aidha, bei ya mafuta kama ilivyoripotiwa mwanzo,
ilikwishaanza kupanda tangu zamani na hata kufikia viwango vya juu kabisa mnamo
mwezi Machi. Kutokana na athari ya vita ya Urusi na Ukraine, bima za vyombo vya
kusafirishia mafuta pia zimepanda kutokana na hatari ya vita hii. Vyombo hivi
pia vinaendeshwa kwa mafuta hayo hayo ambayo yamekwisha panda bei na hivyo
kupelekea gharama zaidi kwa mtumiaji wa mwisho kutokana na gharama za
kuzalisha, kusafisha na kusafirisha bidhaa hii kuwa juu. Gharama hizi zote
wazalishaji huzihamishia kwa watumiaji wa mwisho na kupelekea bei ya mafuta kwa
lita moja (retail price) kupanda.
Kukabiliana
na changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta
Kutokana na athari hizi za vita kati ya Urusi
na Ukraine kwenye bei za mafuta duniani, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania chini ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tayari imekwishaanza
hatua mbalimbali za kifedha kukabiliana na tatizo hili ikiwa ni pamoja na agizo
la Rais kwa serikali kubana matumizi yake ili kuhakikisha fedha kiasi cha
shilingi bilioni 100 zinapatikana kama ruzuku ili kuleta unafuu kwa wananchi
sio tu wanaotumia vyombo vya moto, bali hata kuepusha mfumuko wa bei kwa bidhaa
zingine ambazo zinazalishwa viwandani ambako mafuta pia hutumika kuendeshea
mitambo. Hatua za ziada ikiwemo ruhusa kwa wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei
ya chini kufanya hivyo, kuanzisha mfuko maalumu wa kuhimili ukali wa bei za
mafuta (Fuel Price Stabilization Fund), kuanzisha hifadhi ya mafuta ya
kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve) na zingine kama
alivyowasilisha Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba bungeni, Mei 10
zinaendelea kuchukuliwa na serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata unafuu
licha ya bei kwenye soko la dunia kuzidi kupanda na hivyo kuleta matumaini kwa
wananchi kuepuka hali ngumu za kimaisha ambazo zingetokana na bei kubwa ya
mafuta.
I might say am the biggest fun of these articles i wonder why we lost these potential By the way your article is really inspiring and Keep up the good work I will see you in the Future friend
ReplyDeleteNi vyema kuhabarika juu kile kinachoendelea duniani ili kuwa na tahadhari stahiki na kuweka mikakati ya kukabiliana na matatizo mtambuka yanayotokana na mifarakano baina ya nchi na nchi. Asante kwa uchambuzi wa kina!
ReplyDelete