MIAKA MIWILI TANGU KIFO CHA GEORGE FLOYD: Namna kifo chake kilivyomfanya kuwa alama ya mapambano dhidi ya mauwaji na ubaguzi wa rangi.
Mei 25, 2020, miaka miwili iliyopita, majira ya saa mbili usiku George Perry Floyd Jnr, alinunua pakiti la sigara katika duka linaloitwa Cup Foods katika makutano ya mtaa wa 38 wa Mashariki na mtaa wa Chicago kule Minneapolis, Marekani. Mwajiriwa wa duka lile alimshutumu Floyd kuwa alinunua pakiti lile la sigara kwa noti feki ya $20 na kuamua kumripoti. Baada ya maafisa wa polisi kufika eneo la tukio, walimtia mbaroni Bw. Floyd na kuifunga mikono yake nyuma kwa pingu, kumsogeza kando ya gari lao walipomlaza chini kabla ya afisa mmoja kuamua kumkandamiza shingoni kwa kutumia goti lake mpaka mauti ilipomfika. George Floyd ni moja kati ya mamia, pengine maelfu ya watu waliouwawa kikatili kutokana na ubaguzi wa rangi (racism and white supremacy). Tofauti kubwa ni kwamba, muhanga wa safari hii katika mauwaji ya kikatili yanayosababishwa na dhana za kibaguzi, aliuwawa kikatili huku video iliyoonyesha mauwaji hayo kuanzia alipokamatwa mpaka kifo chake ikizua hisia za huzuni na mshtuko kwa w...