Ugonjwa wa 'Monkeypox': Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi?
‘Monkeypox’ ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho
hutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu (kitaalamu huitwa ‘viral zoonosis’). Huu
ni ugonjwa wenye dalili zinazofanana na zile zilizokuwa zikionekana kwa
wagonjwa wa ndui (smallpox), licha ya kuwa madhara yake mwilini sio makali kama
yale ya ndui. Monkeypox kimsingi ni ugonjwa ambao umekuwepo katika Afrika ya Kati
na Magharibi, sanasana katika maeneo ya misitu ya mvua ya kitropiki na umekuwa
ukisambaa kuelekea maeneo ya mijini.
Jamii kadhaa za wanyama zimetajwa kuathirika zaidi na
kirusi cha ugonjwa huu wa ‘Monkeypox’ ikiwemo aina fulani ya nyani, jamii za
chindi (squirrels), panya kutoka Gambia, na aina zingine kadhaa za wanyama.
Kisa cha kwanza cha Monkeypox kiliripotiwa
mwaka 1970 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mvulana wa miaka tisa
katika kipindi ambacho harakati nyingi sana za kupambana na ugonjwa wa ndui
zilikuwa zikiendelea huku visa zaidi vikiendelea kuripotiwa Afrika ya Kati
Pamoja na Afrika Magharibi. Tangu mwaka 1970, kumeripotiwa visa zaidi katika
nchi takriban 11 barani Afrika huku zaidi ya visa 80 vikiripotiwa katika nchi 9
barani Ulaya na pia Marekani, Canada na Australia. Kisa cha kwanza nchini Uingereza
kiliripotiwa Mei 7 mwaka huu, kwa mgonjwa ambaye alikuwa amerejea nchini humo
kutoka Nigeria ambako wakala wa usalama wa afya nchini Uingereza wanaamini
alipata maambukizi hayo.
Maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu
(zoonotic transmission) yanaweza kutokea kupitia mgusano wa moja kwa moja
(direct contact), damu au aina nyingine za majimaji ya mwilini kutoka kwa
mnyama aliyeathirika. Pia, kula nyama ambayo haijapikwa vizuri au bidhaa za
nyama aina yoyote kutoka kwa mnyama aliyeathirika huweza kuwaweka watumiaji
katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Vilevile, maambukizi kutoka
kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine huweza kutokea kupitia kugusana mwilini na
mgonjwa aliyeathirika, vidonda kwenye ngozi, au kutumia vitu ambavyo mtu
aliyeathirika amevitumia kama vile nguo. Kwa mujibu wa wakala wa afya nchini Uingereza,
ni vigumu sana kwa mtu mwenye kirusi cha ugonjwa wa Monkeypox kumuambukiza mtu
mwingine.
Dalili za ugonjwa huu ni kama vile homa, maumivu ya
kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo, kuvimba kwa tezi na uchovu. Pia,
muathirika huweza kupata upele ambao huweza kuanzia usoni na kusambaa katika
sehemu zingine za mwili. Upele hubadilika na kupitia hatua mbalimbali – hata
kufanana na upele wa ugonjwa wa tetekuwanga – kabla ya kutengeneza kovu ambalo
hufifia na kupotea kabisa. Chunguzi mbalimbali za kisayansi zimeainisha kuwa
dalili za ugonjwa huu sio kali sana na huisha baada ya wiki mbili mpaka nne.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa tamko rasmi
kuhusiana na ugonjwa huu Mei 19 2022. Katika tamko hilo, Shirika la Afya Duniani
limeainisha kuwa, kutambulika kwa makundi ya visa vya Monkeypox mwezi Mei 2022
katika maeneo ambayo hayana muunganiko wa moja kwa moja kwa njia za usafiri ni
hali isiyo ya kawaida. Aidha, uchunguzi zaidi unaendelea ili kuweza kubainisha
chanzo na ukomo wa milipuko hii katika siku zijazo. Pia, shirika hilo
limependekeza kuwa wakati uchunguzi unaendelea, ni vyema kuendelea kuzingatia njia
zote ambazo maambukizi ya ugonjwa huu huenda yakapitia ili kuilinda jamii dhidi
ya milipuko zaidi. Kwa muda sasa, maambukizi yametokana na kusambaa kwa virusi
kutoka kwa wanyama walioathirika kwenda kwa binadamu. Kugusana na wanyama bila
ya kujikinga au bila kuchukua tahadhari, hasa wale ambao wana maambukizi ya
virusi hivi, wanaoumwa au waliokufa ikiwemo nyama yao, damu na sehemu zingine
za mwili ni vyema vikaepukwa. Kwa kuongezea, vyakula aina zote za nyama au viungo
vya wanyama ambavyo hutumika kama chakula ni vyema vikapikwa vizuri kabla ya
kuandaliwa mezani.
Kwa sababu ya utandawazi, hakuna jambo kubwa ambalo
litatokea katika sehemu moja ya dunia bila kuleta mtikisiko au athari fulani
katika sehemu nyingine, iwe ni moja kwa moja au kwa namna isiyo ya moja kwa
moja. Kuripotiwa kwa visa vya ugonjwa huu katika nchi za Ulaya kunatakiwa kuwe sababu
kwa nchi zote duniani ikiwemo Tanzania kuanza kujiandaa na kupeana elimu juu ya
ugonjwa huu. Ushahidi wa wazi ni kisa cha kwanza kilichoripotiwa Uingereza
ikiaminika muathirika alitoka safari nchini Nigeria. Nchini Australia pia, kisa
cha kwanza kuripotiwa ni kwa mtu aliyeanza kuumwa baada ya kutoka safari nchini
Uingereza. Hii ni kwa visa vilivyoripotiwa. Kwa mantiki hii, ni wazi kuwa hakuna
nchi iliyo salama kabisa na huenda ni suala la muda tu kabla visa zaidi
havijaripotiwa katika nchi mbalimbali, Tanzania ikiwemo.
Kuwa na wasiwasi pekee haitosaidia bali yatupasa sote
kujiandaa kiakili na kimazingira na kuanza kuchukua tahadhari kadri tuwezavyo
ikiwemo kuripoti dalili zozote za ugonjwa huu, kuepuka misongamano isiyo ya
lazima, upishi mzuri wa nyama na kuepuka kuchangia vitu kama nguo ili kuepusha
mlipuko wa ugonjwa huu nchini mwetu.
Mungu akubariki kwa uchambuzi mzuri.
ReplyDelete