Ugonjwa wa 'Monkeypox': Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi?

‘Monkeypox’ ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho hutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu (kitaalamu huitwa ‘viral zoonosis’). Huu ni ugonjwa wenye dalili zinazofanana na zile zilizokuwa zikionekana kwa wagonjwa wa ndui (smallpox), licha ya kuwa madhara yake mwilini sio makali kama yale ya ndui. Monkeypox kimsingi ni ugonjwa ambao umekuwepo katika Afrika ya Kati na Magharibi, sanasana katika maeneo ya misitu ya mvua ya kitropiki na umekuwa ukisambaa kuelekea maeneo ya mijini.

Jamii kadhaa za wanyama zimetajwa kuathirika zaidi na kirusi cha ugonjwa huu wa ‘Monkeypox’ ikiwemo aina fulani ya nyani, jamii za chindi (squirrels), panya kutoka Gambia, na aina zingine kadhaa za wanyama.

Kisa cha kwanza cha Monkeypox kiliripotiwa mwaka 1970 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mvulana wa miaka tisa katika kipindi ambacho harakati nyingi sana za kupambana na ugonjwa wa ndui zilikuwa zikiendelea huku visa zaidi vikiendelea kuripotiwa Afrika ya Kati Pamoja na Afrika Magharibi. Tangu mwaka 1970, kumeripotiwa visa zaidi katika nchi takriban 11 barani Afrika huku zaidi ya visa 80 vikiripotiwa katika nchi 9 barani Ulaya na pia Marekani, Canada na Australia. Kisa cha kwanza nchini Uingereza kiliripotiwa Mei 7 mwaka huu, kwa mgonjwa ambaye alikuwa amerejea nchini humo kutoka Nigeria ambako wakala wa usalama wa afya nchini Uingereza wanaamini alipata maambukizi hayo.

Maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu (zoonotic transmission) yanaweza kutokea kupitia mgusano wa moja kwa moja (direct contact), damu au aina nyingine za majimaji ya mwilini kutoka kwa mnyama aliyeathirika. Pia, kula nyama ambayo haijapikwa vizuri au bidhaa za nyama aina yoyote kutoka kwa mnyama aliyeathirika huweza kuwaweka watumiaji katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Vilevile, maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine huweza kutokea kupitia kugusana mwilini na mgonjwa aliyeathirika, vidonda kwenye ngozi, au kutumia vitu ambavyo mtu aliyeathirika amevitumia kama vile nguo. Kwa mujibu wa wakala wa afya nchini Uingereza, ni vigumu sana kwa mtu mwenye kirusi cha ugonjwa wa Monkeypox kumuambukiza mtu mwingine.

Dalili za ugonjwa huu ni kama vile homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo, kuvimba kwa tezi na uchovu. Pia, muathirika huweza kupata upele ambao huweza kuanzia usoni na kusambaa katika sehemu zingine za mwili. Upele hubadilika na kupitia hatua mbalimbali – hata kufanana na upele wa ugonjwa wa tetekuwanga – kabla ya kutengeneza kovu ambalo hufifia na kupotea kabisa. Chunguzi mbalimbali za kisayansi zimeainisha kuwa dalili za ugonjwa huu sio kali sana na huisha baada ya wiki mbili mpaka nne.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa tamko rasmi kuhusiana na ugonjwa huu Mei 19 2022. Katika tamko hilo, Shirika la Afya Duniani limeainisha kuwa, kutambulika kwa makundi ya visa vya Monkeypox mwezi Mei 2022 katika maeneo ambayo hayana muunganiko wa moja kwa moja kwa njia za usafiri ni hali isiyo ya kawaida. Aidha, uchunguzi zaidi unaendelea ili kuweza kubainisha chanzo na ukomo wa milipuko hii katika siku zijazo. Pia, shirika hilo limependekeza kuwa wakati uchunguzi unaendelea, ni vyema kuendelea kuzingatia njia zote ambazo maambukizi ya ugonjwa huu huenda yakapitia ili kuilinda jamii dhidi ya milipuko zaidi. Kwa muda sasa, maambukizi yametokana na kusambaa kwa virusi kutoka kwa wanyama walioathirika kwenda kwa binadamu. Kugusana na wanyama bila ya kujikinga au bila kuchukua tahadhari, hasa wale ambao wana maambukizi ya virusi hivi, wanaoumwa au waliokufa ikiwemo nyama yao, damu na sehemu zingine za mwili ni vyema vikaepukwa. Kwa kuongezea, vyakula aina zote za nyama au viungo vya wanyama ambavyo hutumika kama chakula ni vyema vikapikwa vizuri kabla ya kuandaliwa mezani.

Kwa sababu ya utandawazi, hakuna jambo kubwa ambalo litatokea katika sehemu moja ya dunia bila kuleta mtikisiko au athari fulani katika sehemu nyingine, iwe ni moja kwa moja au kwa namna isiyo ya moja kwa moja. Kuripotiwa kwa visa vya ugonjwa huu katika nchi za Ulaya kunatakiwa kuwe sababu kwa nchi zote duniani ikiwemo Tanzania kuanza kujiandaa na kupeana elimu juu ya ugonjwa huu. Ushahidi wa wazi ni kisa cha kwanza kilichoripotiwa Uingereza ikiaminika muathirika alitoka safari nchini Nigeria. Nchini Australia pia, kisa cha kwanza kuripotiwa ni kwa mtu aliyeanza kuumwa baada ya kutoka safari nchini Uingereza. Hii ni kwa visa vilivyoripotiwa. Kwa mantiki hii, ni wazi kuwa hakuna nchi iliyo salama kabisa na huenda ni suala la muda tu kabla visa zaidi havijaripotiwa katika nchi mbalimbali, Tanzania ikiwemo.

Kuwa na wasiwasi pekee haitosaidia bali yatupasa sote kujiandaa kiakili na kimazingira na kuanza kuchukua tahadhari kadri tuwezavyo ikiwemo kuripoti dalili zozote za ugonjwa huu, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, upishi mzuri wa nyama na kuepuka kuchangia vitu kama nguo ili kuepusha mlipuko wa ugonjwa huu nchini mwetu.

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

MFUMUKO WA BEI YA MAFUTA: Namna vita ya Urusi na Ukraine inavyochangia kupanda kwa bei ya mafuta na hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na mfumuko huo nchini Tanzania.

MALKIA ELIZABETH II