MIAKA MIWILI TANGU KIFO CHA GEORGE FLOYD: Namna kifo chake kilivyomfanya kuwa alama ya mapambano dhidi ya mauwaji na ubaguzi wa rangi.
Mei 25, 2020, miaka miwili iliyopita, majira
ya saa mbili usiku George Perry Floyd Jnr, alinunua pakiti la sigara katika
duka linaloitwa Cup Foods katika makutano ya mtaa wa 38 wa Mashariki na mtaa wa
Chicago kule Minneapolis, Marekani. Mwajiriwa wa duka lile alimshutumu Floyd
kuwa alinunua pakiti lile la sigara kwa noti feki ya $20 na kuamua kumripoti. Baada
ya maafisa wa polisi kufika eneo la tukio, walimtia mbaroni Bw. Floyd na kuifunga
mikono yake nyuma kwa pingu, kumsogeza kando ya gari lao walipomlaza chini
kabla ya afisa mmoja kuamua kumkandamiza shingoni kwa kutumia goti lake mpaka
mauti ilipomfika.
George Floyd ni moja
kati ya mamia, pengine maelfu ya watu waliouwawa kikatili kutokana na ubaguzi
wa rangi (racism and white supremacy). Tofauti kubwa ni kwamba, muhanga wa
safari hii katika mauwaji ya kikatili yanayosababishwa na dhana za kibaguzi, aliuwawa
kikatili huku video iliyoonyesha mauwaji hayo kuanzia alipokamatwa mpaka kifo
chake ikizua hisia za huzuni na mshtuko kwa watu duniani kote. Video hii
ilirekodiwa na binti wa miaka 17 aitwaye Darnella Frazier kwa simu yake ya
mkononi na baadaye kusambaa mtandaoni. Mauwaji haya yalizua taharuki na kuleta
hamasa zaidi kwa muendelezo wa kauli mbiu maarufu ya kupinga unyanyasaji na
ukosefu wa usawa kati ya watu wenye ngozi ya rangi nyeusi na nyeupe ambayo
inafahamika kama ‘Black Lives Matter’ iliyoanzishwa na mabinti watatu baada ya mauwaji
mengine ya kikatili ya kijana wa miaka 17, Trayvon Martin aliyepigwa risasi na
jirani yao, George Zimmerman. Mbali na mchango mkubwa wa mitandao ya kijamii
katika kuamsha hisia za watu na utambuzi juu ya ukatili wa polisi kwa Wamarekani
weusi, uuwaji wa George Floyd pia ulikua wa kikatili sana. Askari polisi aliyesababisha
kifo chake alimkandamiza shingoni kwa muda usiopungua dakika 8 na sekunde 46
huku Floyd akihangaika sana na kusema “siwezi kupumua” mara 16. Licha ya George
Floyd kulalamika sana, afisa aliendelea kumkandamiza mpaka alipopoteza uhai
wake. Uchunguzi zaidi uliofanywa na daktari wa kituo cha matibabu cha Hennepin
ambako George Floyd aliwahishwa haukubainisha ushahidi wowote wa shinikizo la
kubanwa kifua au kunyongwa hivyo pengine vichocheo fulani katika mfumo wake na
kukandamizwa na afisa kulichangia kifo chake iliripoti BBC.
Moja kati ya kanuni za
msingi ambazo zinalijenga taifa la Marekani ni pamoja na haki, usawa na uhuru
wa kujieleza lakini kwa vizazi vingi sasa Wamarekani weusi wamekuwa wakihisi
ukosefu wa usawa (wakionewa) huku hali hii ikiwafanya wakumbuke kipindi cha
ukatili wa kitumwa. Badala ya kuangaliwa kwa uhalisia na hoja stahiki za kihistoria,
wazawa wa Afrika na watu wenye ngozi nyeusi wameelezewa kwa mtazamo wa kimashariki
zaidi ambao hutizama Waafrika au watu wenye asili ya Afrika kama walimbukeni,
waliokosa elimu, wasiostarabika, masikini, tegemezi na wavamizi. Ni jambo linalostaajabisha
wengi kuwa watu walioleta watumwa kutoka nyumbani kwao pa asili, wakaishi
katikati yao (japo kama watumwa) na kuzaliana nao, leo wanawabagua na kuwaona
wavamizi.
Tangu miaka ya 1960
kumekuwa na madai mengi ya haki na usawa nchini marekani kwa watu Weusi. Mwaka
1991 Rodney King, pia Mmarekan mweusi alipigwa kikatili na maafisa wa polisi wa
Los Angeles baada ya kukamatwa sababu ya uendeshaji wa kasi. Mwezi Julai 2014
baba wa watoto 6 Eric Garner pia alifanyiwa ukatili na askari polisi
uliosababisha kifo chake baada ya kutuhumiwa kuuza sigara moja kutoka kwa
pakiti bila stempu za ushuru. Mauwaji
haya yote yalileta na yanaendelea kuleta taharuki huku waandamanaji mbalimbali pia
wakikamatwa na kufungwa kutokana na vurugu kusemwa ‘zimepitiliza’ na mamlaka
husika katika nyakati tofautitofauti. Mbali zaidi, baadhi ya waandishi wa
habari pia wamekuwa wakikamatwa ilihali wakiwa wanajaribu tu kuionyesha dunia
yale yanayoendelea. Watu mashuhuri kama Malcom X na Martin Luther King waliodai
haki na usawa kutoka kwa ndugu ambao wanatofautiana tu rangi ya ngozi waliuwawa
katika kutetea usawa huu.
Derek Chauvin, askari
aliyesababisha kifo cha George Floyd alihukumiwa miaka 22 na miezi 6 jela, Juni
26, 2021 kwa mauwaji ya shahada ya pili na mashtaka mengine huku jaji akisema kuwa
hukumu yake imetokana pia na unyanyasaji wake, matumizi mabaya ya wadhifa, na
vilevile ukatili alioonesha kwa Floyd. Inadaiwa Chauvin alikwishalalamikiwa zaidi
ya mara 12 katika muda wake wote wa uzoefu wa kazi kwa zaidi ya miaka 18 kuhusu
kukiuka taratibu za kazi yake, iliripoti SkyNews katika Makala yake ya ‘8
Minutes and 46 Seconds - The Killing of George Floyd’. Mama wa Derek Chauvin, Carolyn
Pawlenty alisema mahakamani kuwa, “Daima ninaamini kuwa huna hatia na
sitabadili mtazamo wangu.” Askari polisi wengine watatu waliohusika na tukio la
mauwaji ya George Floyd walikutwa na hatia ya makosa ya unyanyasaji na kusaidia
mauwaji ya shahada ya pili.
Kumekuwa na wasiwasi
kuwa huenda mzunguko na marudio ya matatizo yote haya ya unyanyasaji na mauwaji
yanayofanywa na askari polisi dhidi ya Wamarekani weusi hauna mwisho. Wengi hudhani
kuwa biashara ya utumwa ndiyo dhambi asilia iliyosababisha karne nyingi za
mateso na ukosefu wa usawa kwa Wamarekani Weusi; ikiwa kuna ukweli wowote
katika hili, basi watu hawa wanateseka kwa makosa ambayo hawakuyafanya. Kwa
muda sasa, yaonekana kuwa kupata suluhu, ufumbuzi au njia thabiti za kudhibiti
makosa haya ya ubaguzi wa rangi yaliyoenda mbali zaidi na kufikia hatua ya
kuuwawa kwa raia wasio na hatia imeshindikana. Baada ya mauwaji ya George
Floyd, watu wengi walishauri kuwa ufike wakati ambao askari polisi watanyang’anywa
nguvu na vyeo walivonavyo ndipo masuala ya ukatili dhidi ya watu wenye ngozi
nyeusi utaisha. Hata hivyo, meya wa Minneapolis wakati ule wa mauwaji ya George
Floyd alisema kuwa itakuwa ngumu kuondoa kabisa polisi ambao kazi yao ni
kulinda raia na mali zao lakini ilikuwa dhahiri kuwa mabadiliko katika jeshi la
polisi yanahitajika.
Safari ya ubaguzi wa
rangi imekuwa ni ndefu. Mpaka kufika sasa, wakati wa utandawazi, wakati ambao
watu wengi wameelimika na kupata utashi wa kutosha kustaarabika na kutambua
haki za binadamu ambazo hazibagui na hazichagui, ni jambo la kushangaza kuona
watu wanabaguana na kuuana kwa sababu tu rangi za ngozi zao zinatofautiana.
Kulikuwa na wakati ambao watu weusi nchini Marekani waliishi kwa hofu katika
nchi hiyohiyo ambayo wao ni wazawa na pengine hadi sasa, baadhi wana hofu hiyo;
nyakati ambazo mauwaji yangetokea na yasingeripotiwa sehemu yoyote wala
kufahamika kwa watu. Kifo cha George Floyd, aliyekuwa baba wa watoto watano,
kimekuwa kichocheo, jiwe kuu la pembeni katika kujenga dunia na kuleta mwamko
na pengine mwanzo wa ukingo wa kuelekea kuondokana na tatizo hili. Aidha,
matumaini kama haya yalishakuwepo awali; mfano mwaka 2009 baada ya nchi ya
Marekani kupata rais wa kwanza mweusi, wengi walidhani huenda walishaona mateso
ya mwisho ya aina hii kwa Wamarekani weusi lakini mauwaji haya yaliendelea
kutokea. Licha ya ishara zote kuwa dunia inaenda katika uelekeo sahihi hasa
baada ya mauwaji yan George Floyd kuonekana wazi, bado mwisho rasmi wa mauwaji na
ubaguzi huu uko zaidi ya upeo wa macho na hata utabiri. Hata hivyo, kifo cha
George Floyd kitabaki kuwa alama katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Chaguzi ingekuwa kwa dunia, basi hakika dunia ingechagua George Floyd aendelee
kuishi maisha yake kwa amani, kuwalea watoto wake na kutimiza kikamilifu yale
ambayo hakutimiza. Kama ni alama ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na
ukatili wa polisi, basi ingetafutwa alama nyingine. Lakini yaliyotokea
yametokea; apumzike kwa amani, George Perry Floyd Jnr.
Kunyanyaswa kwa Watu Weusi nchini Marekani ni mkakati wa kimfumo ambao umekuwapo
ReplyDeletekwa miaka mingi ukiwa na lengo la kuhakikisha hawapati fursa maridhawa sawia na Wazungu hivi kwamba nao wakaweza kuwa jamii yenye ustawi mujarabu - kimsingi, ni kama bado vidonda vyao vya utumwa vikiwa vinatoneshwa!