SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022

 Sensa ya watu na makazi ni nini?

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathmini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemografia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalumu. Ifikapo Agosti 23 mwaka huu, Sensa ya watu na makazi itafanyika nchini, ikiwa ni Sensa ya sita (Sensa zingine zilikuwa katika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002, na 2012), Sensa ambazo hufanyika kila baada ya miaka kumi. Serikali imekuwa ikihamasisha na kuweka juhudi kubwa katika kuhakikisha watu wanajiandaa na wanajitokeza kwa wingi kuhesabiwa. Mnamo tarehe 08 mwezi Aprili mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, alitoa agizo kwa viongozi kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi ili wajitokeze na kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi wakati akizindua Nembo na tarehe ya Sensa ya mwaka 2022 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar. Serikali pia imeendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi wote kwa kuweka mabango katika baadhi ya sehemu yenye kukumbushia watu kuwa tayari na matumizi ya nembo ya Sensa kwenye nyaraka zake mbalimbali.

Kwanini serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhamasisha watu kuhesabiwa? Kuna faida gani?

Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Mtawala Kata ya Mwembesongo mkoani Morogoro, kamisaa wa Sensa kitaifa ambaye pia ni Spika wa Bunge Mstaafu Bi. Anne Makinda, Septemba Mosi mwaka 2021 aligusia kuwa Sensa itaisaidia serikali kutambua matumizi bora ya kodi zinazotolewa na wananchi. Mfano wa kuelezea zaidi umuhimu huu, upo katika Maisha yetu ya kila siku hasa katika ngazi za kaya au familia. Fikiria, mtu yeyote aliye na familia huanza kwanza kwa kutambua idadi ya wanafamilia, umri wao, mahitaji yao kulingana na umri, huangalia mahali wanapoishi na gharama za kimaisha katika eneo hilo, kisha hupangilia bajeti yake na namna atakavyogawa kipato chake ili kuhakikisha anatimiza mahitaji ya kila mmoja katika familia yake. Hivi ndivyo inavyotakiwa tulifikirie taifa hili ambalo linaongozwa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita. Sensa pia itaisaidia Serikali kuapata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

 Ni jambo la umuhimu mkubwa kwa serikali kujua idadi ya watu wote, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo, hali ya makazi na makundi yenye uhitaji maalumu. Kama ilivyo katika ngazi ya familia, kujua idadi ya watu na taarifa zinazowahusu itaisaidia familia hii kubwa zaidi, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia serikali yake kupanga mipango ya kimaendeleo ambayo itaakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali ikiwemo namna kodi itakavyotumika kwenye kusaidia maisha ya watanzania ambao kodi hizi hukusanywa kwao kuwa mazuri.

Sensa ya Watu na Makazi pia ina mchango mkubwa katika kuimarisha msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia ya uwakilishi. Takwimu sahihi za Sensa zihatajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 75(3) na (4) imeainisha vigezo vinavyohusika katika ugawaji wa majimbo ya uchaguzi. Idadi ya watu katika eneo lililokusudiwa ni moja ya vigezo hivyo. Vilevile, takwimu za Sensa zitaisaida serikali kujua kasi ya ukuaji wa idadi ya watu ili kuweza kujipanga kujua namna ya kukabiliana na changamoto za kimazingira zitokanazo na idadi ya watu nchini ikiwa ni katika kuendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG au Ajenda 2030) ya Umoja wa Mataifa (UN).

Takwimu za Sensa pia hutumiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, watafiti, taasisi mbalimbali na wawekezaji katika kupanga shughuli zao. Hii ni moja ya sababu Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Alibina Chuwa alisisitiza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yana nafasi kubwa katika kusaidia kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki kwenye zoezi la Sensa. Dkt. Chuwa aliyasema haya wakati akizungumza kwenye kikao kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali. Ni Dhahiri kuwa, mfanyabiashara yeyote huangalia kwanza idadi ya watu au mzunguko wa watu kabla ya kuamua kuanza shughuli zake za kibiashara katika eneo husika. Vivyo hivyo kwa wawekezaji na mashirika yasiyo ya kiserikali na hata ya kiserikali ambayo hutoa huduma mbalimbali za kijamii.

Imani potofu kuhusu Sensa na uhalisia wa mambo

Dhana zisizo za kweli kuhusu Sensa ambazo ziko miongoni mwa baadhi ya wananchi ni moja ya sababu za serikali kutumia juhudi kubwa kuhamasisha watu kushiriki katika zoezi hili. Baadhi ya watu huamini kuhesabu idadi ya watoto huleta mikosi katika familia. Wengine wamekuwa wakihusisha Sensa na Chanjo ya UVIKO-19, kwamba inalenga kujua idadi ya watanzania waliochanjwa na wale ambao hawajachanjwa, jambo ambalo si kweli kabisa. Sensa haihusiani kabisa na chanjo ya UVIKO-19 ingawa kupata chanjo hiyo ni muhimu katika kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo. Katika Taarifa kwa vyombo vya Habari iliyotolewa Aprili 8 mwaka huu na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Mhe. Samia Suluhu Hassan pia alieleza kuwa mwenendo wa baadhi ya jamii au familia kuwaficha na kuwazuia watu wenye ulemavu kutoshiriki katika kuhesabiwa ni kinyume na haki za binadamu.

Sensa ya Watu na Makazi 2022 itafanyika vipi na ni vitu gani vya kufahamu kuihusu?

Siku ya sensa, karani wa Sensa akiongozana na Mwenyekiti au kiongozi wa Serikali ya Mtaa au Kitongoji atafika katika kaya akiwa na kitambulisho cha Karani wa Sensa na Dodoso la Sensa lililowekwa katika kifaa cha kielektroniki kiitwacho kishikwambi (Tablet) na kuuliza maswali ambayo yatajibiwa na Mkuu wa kaya. Ikiwa mkuu wa kaya hatokuwepo, mtu mwingine yeyote mzima katika kaya ambaye atakuwa na taarifa za kutosha kuhusiana na kaya na wote waliolala ndani ya kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa ataweza kujibu maswali ya Sensa kwa niaba yake. Kwa mujibu wa sheria ya Takwimu sura ya 351, ni wajibu wa mhusika kujibu maswali ya Sensa. Kwa mujibu wa Sheria hii pia, taarifa zote zitakazotolewa kwa karani zitakuwa SIRI na zitatumika kwa madhumuni ya kitakwimu pekee. Chini ya sheria hii, kila karani atasaini kiapo cha kutunza siri za taarifa zote atakazokusanya, taarifa ambazo zitawasilishwa katika Ofisi ya Taifaa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS) tu. Baadhi ya taarifa zitakazokunywa ni kama taarifa za kidemografia (umri, jinsi, hali ya ndoa), ulemavu, uhamaji, vitambulisho ya utaifa, elimu, shughuli za kiuchumi, vifo, umiliki wa ardhi, makazi, nyumba, umiliki wa nyumba, hali za uzazi, TEHAMA, taarifa za kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na huduma za kijamii katika ngazi ya kitongoji/shehia na mitaa.

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ni sehemu ya msingi bora wa kujenga Tanzania imara.

Nikihesabiwa, ukihesabiwa, akihesabiwa na wakihesabiwa, sote tutakuwa tumehesabiwa.

Sensa kwa Maendeleo,

Jiandae Kuhesabiwa.


Comments

Popular posts from this blog

MFUMUKO WA BEI YA MAFUTA: Namna vita ya Urusi na Ukraine inavyochangia kupanda kwa bei ya mafuta na hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na mfumuko huo nchini Tanzania.

Ugonjwa wa 'Monkeypox': Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi?

MALKIA ELIZABETH II