MALKIA ELIZABETH II
Uingereza leo hii, baada ya zaidi ya miaka 70 imeshuhudia kuchomoza kwa jua pasi na Malkia Elizabeth II kuwa kwenye utawala. Mnamo Septemba 9 2022, Malkia Elizabeth II aliyedumu muda mrefu zaidi nchini humo alifariki akiwa Balmoral akiwa na umri wa miaka 96 baada ya kutawala kwa zaidi ya maiak 70. Hakuna kiongozi aliyewahi kuwa na uzoefu kama huu. Mamilioni ya watu duniani wameungana na Waingereza na watu wa mataifa mengine 14 aliyokuwa akitawala mpaka umauti ulipomfika katika kuomboleza kifo cha Malkia Elizabeth II. Malkia Elizabeth II ni nani has ana kwanini kifo chake kimewagusa wengi?
Wasifu wa Malkia Elizabeth na historia ya maisha yake
Elizabeth Alexandra Mary Windsor alizaliwa mnamo Aprili 21, 1926 katika jumba lililokuwa karibu na Berkeley Square jijini London. Alikuwa mtoto wa kwanza wa Albert, mwanamfalme Mtawala wa York na mkewe ambaye zamani alifahamika kama Lady Elizabeth Bowes-Lyon. Elizabeth na dada yake Margaret Rose (aliyezaliwa 1930) walilelewa katika mazingira ya familia yenye upendo, na licha ya kutohudhuria masomo katika shule ya kawaida, Elizabeth alifanya vyema sana katika kuzifahamu lugha mbalimbali na alifanya usomaji wa kina wa historia ya kikatiba. Alipokuwa na miaka sita, Elizabeth alimwambia mwalimu wake wa uendeshaji farasi kuwa alitaka kuwa “mwanamke wa kukaa mashambani na awe na farasi na mbwa wengi.” Hii inaweza kuelezea mapenzi yake ya kufanya likizo sehemu za nje ya miji na mashambani hasa katika majira ya kiangazi. Watu wachache sana walitabari kuwa huenda Elizabeth angekuja kuwa malkia.
Mwaka 1936, mjomba wake Elizabeth, Edward VIII alijiondoa kwenye kiti cha ufalme na kuoana na MMarekani aliyewahi kutalikiana mara mbili, Wallis Simpson, jambo mbalo lilikuwa kinyume na tamaduni za Waingereza. Baada ya kufikisha umri wa miaka 18, Elizabeth alitumia muda wa miezi mitano kwenye huduma za usaidizi wa jeshi na kujifunza ufundi wa msingi wa magari na ustadi wa kuendesha. Elizabeth alikuwa na uhusiano wa karibu sana na babu yake Josh V pamoja na baba yake. Uhusiano wa karibu kati ya baba yake na watu wake ulimfurahisha sana Elizabeth kiasi akaapa siku aliyotimiza miaka 21 kwa kusema kwa watu, “Ninasema mbele yenu kuwa hata unywele wangu ukiwa mrefu au mfupi, nitajitoa kuwahudumia na kuihudumia familia yetu ya kifalme ambayo ni ya kwetu sote.” Mnamo tarehe 20 Novemba 1947, Malkia Elizabeth alifunga ndoa na Prince Philip, Duke wa Edinburg baada ya miezi kadhaa ya uchumba na baadaye kupata Watoto wanne, Charles, Anne, Andrew na Edward.
Ilipofika mwaka 1952, baba yake Elizabeth George VI alifariki dunia baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu. Moja kwa moja, Elizabeth alipaswa kutawazwa kuwa Malkia wa Uingereza. Hata hivyo, kutokana na heshima aliyokuwa nayo kwa baba yake, Elizabeth alisubiri miezi 16 ipite ndipo alipokuja kutawazwa mwaka 1953, Westminister Abbey, huku tukio hilo likirushwa kwenye vyombo vya Habari na mamilioni ya watu duniani kulishuhudia.
Katika kipindi cha utawala wake, Malkia Elizabeth II alikuwa na jumla ya mawaziri wakuu 14 aliowahi kufanya nao kazi, wa kwanza akiwa ni Winston Churchill (1951-55), rafiki yake mkubwa ambaye aliwahi kukaririwa akisema kuwa Elizabeth alionyesha sifa za uongozi na kupenda kuongoza tangu alipokuwa na umri mdogo sana. Nicholas Soames, mjukuu wa Churchill pia amewahi kukaririwa akisema kuwa Malkia alimuheshimu sana babu yake kutokana na uzoefu aliokuwa nao.
Utawala wa Malkia Elizabeth II; milima na mabonde
Licha ya kuwa kiongozi wa dola, Malkia hutakiwa kutawala pasi na kuunga mkono au kuhusika na mlengo wowote wa kisiasa. Licha ya kuwa yeye ndiye huvaa taji la kifalme, nguvu ya kisiasa kaika himaya yake hushikwa na wengine. Uwezo wa kipekee wa Malkia Elizabeth II wa kujitenga kabisa na ushawishi wowote wa kisiasa hutajwa kama moja ya sababu ya kukaa kwake madarakani kwa mrefu kuliko kiongozi mwingine yeyote katika nafasi yoyote duniani. Ni ngumu sana kumfikiria au kutabiri msimamo wa kiongozi wa aina hii, kiongozi asiyefanya mahojiano yoyote na kipindi chochote cha luninga wala magazeti. Mfano, watu wengi walihoji msimamo wa Malkia Elizabeth II kuhusu suala la Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (BRExit) bila kuoata majibu. Waliomtangulia Malkia Elizabeth II katika utawala wao walikuwa wakihusika moja kwa moja katika masuala ya kisiasa hasa ufanyaji maamuzi na masuala ya sera za mambo ya nchi. King John, mathalani, alitumia fedha na mali nyingi wakati wa utawala wake kushiriki katika vita huku Malkia Elizabeth I alikuwa mtawala aliyejihusisha kwa upana na masuala ya kisiasa hadi kufikia katika ngazi ya bara.
Mawaziri wakuu nchini Uingereza, kiutaratibu huwa na kikao au huripoti kwa Malkia kila wiki. Mkuu asiye na makuu, Malkia Elizabeth II aliaminika kuwa kiongozi asiyependa mafarakano wala kutokubaliana na wale chini yake. Aidha, katika nyakati mbalimbali, baadhi ya mawaziri wakuu hawakuwa na mitazamo sawa na Malkia Elizabeth II kuhusu mambo Fulani. Mfano ni Margaret Thatcher, Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Uingereza aliyekuwa madarakani mwaka 1979 mpaka 1990. Nchi za Jumuiya ya Madola ziliwasilisha maombi kwake kuwa achukue upande dhidi ya Apartheid Policy (Sera ya kibaguzi nchini Afrika Kusini), lakini alikataa kujihusisha kabisa na matatizo aliyodai kuwa ‘hayamuhusu’. Hata ilipofika bungeni, Waziri Mkuu huyu aliweka vizingiti vya suala hili kuzungumziwa. Malkia Elizabeth II hakuridhishwa na upuuziaji huu. Kama ilivyo hulka yake ya kuepusha mafarakano, Malkia Elizabeth II alisafiri bila kumtaarifu Waziri Thatcher na kwenda kuhudhuria mkutano wan chi hizo za Jumuiya ya Madola juu ya namna ya kuweka vikwazo ili kuondosha sera hii ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Jambo hili lilimjengea heshima kubwa zaidi Malkia Elizabeth II katika jumuiya ya kimataifa hasa katika nchi ambazo ni wanajumuiya ya Jumuiya ya Madola.
Mwaka 1992 haukuwa mwaka mzuri kwa utawala wa Malkia Elizabeth II. Malkia mwenyewe aliuita ‘annus horribilis’ akimaanisha mwaka wa majanga. Hiki kilikuwa ni kipindi cha maumivu kwake yeye binafsi, kwa familia yake na kwa utawala wake. Kulizuka moto ulioharibu Windsor Castle, jumba la kifalme la familia na ndoa tatu za Watoto wake zilivunjika. Wengi walidhani pengine huu ndiyo ungekuwa mwisho wa utawala wa Malkia Elizabeth II, ambaye alikuwa akitupiwa lawama na vyombo vya Habari hasa magazeti kuwa huenda yeye ndiye chanzo cha matatizo ya ndoa za Watoto wake. Wengi walihoji kama alifaa kubaki kwenye kiti kutokana na skendo nyingi zilizoihusisha familia yake. Hata hivyo Malkia alibaki kuwa mtulivu huku akitanguliza wajibu wake kwa jamii na kuyatatua matatizo ya kifamilia nyuma ya pazia kadiri ilivyowezekana. Aliwatanguliza Waingereza kabla ya familia yake.
Malkia Elizabeth II alikumbwa na na janga jingine pale alipompoteza mwanae wa kike Princess Diana aliyefariki katika ajali ya gari. Princess Diana aliacha Watoto wawili, wajukuu wa Malkia Elizabeth II ambao ndio aliwafikiria sana baada ya kupata taarifa ile ya kifo alipokuwa mapumzikoni. Malkia Elizabeth II aliamuru wajukuu wake wawekwe mbali na vyanzo vyote vya habari. Pengine Malkia Elizabeth II aliitanguliza familia yake kabla ya wananchi wa Uingereza ambao wote waliomboleza kifo cha Princess Diana kwani alipendwa sana na watu. Malkia hakutoka kuongea na watu wake mpaka zilipopita siku tano. Katika kipindi hicho, wengi walihoji kwanini Malkia hakuungana nao kuomboleza mapema na kuwa huenda wakati umefika majukumu yake yamemuelemea. Lakini kwa upande mwingine, baadhi walielewa kuwa Malkia Elizabeth II licha ya utawala wake, alikuwa ni binadamu, mama ambaye alikuwa amempoteza mtoto wake. Hata hivyo baada ya hotuba yake siku tano baada ya kifo cha binti yake, watu walirudisha mioyo yao kwake.
Katika milima na mabonde yote kwenye utawala wa Malkia Elizabeth, Duke wa Edinburgh na mume wa Malkia Elizabeth II, Prince Philip alikuwa kando ya mke wake kwa zaidi ya miongo sita ya utawala wake na mnamo mwaka 2009 alikuwa mume aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Uingereza. Baada ya changamoto na mabonde mengi aliyopitia Malkia Elizabeth II, bonde kubwa pengine kuliko yote lilikuwa bado kumfika. Aprili 9 mwaka 2021 Prince Philip alifariki dunia. Licha ya kifo cha mume wake, Malkia Elizabeth II aliendelea kuonyesha ushupavu. Kipindi hiki ni dhahiri kuwa kilikuwa kigumu kwa Malkia Elizabeth II kama ambavyo kingekuwa kigumu kwa binadamu yeyote ambaye angekuwa katika nafasi yake. BRExit, UVIKO-19, mwanae kujitenga na familia yao ya kifalme, kifo cha mumewe ni changamoto zilizomuandama kama kiongozi, kama mke na kama mama, zote kwa pamoja. Hata hivyo, aliendelea kutunza kiapo chake cha kutumikia watu wake nyakati zote. Wiki kadhaa tu baada ya kifo na msiba wa mumewe, Malkia Elizabeth II alirudi katika shughuli zake za kijamii na miezi miwili baaadaye alishiriki kwenye ufunguzi wa kikao cha wakuu wa nchi kuu saba (G7 Summit).
Nini kinafuata baada ya kifo cha Malkia Elizabeth II
Katika kipindi cha utawala wake, Malkia Elizabeth II alihutubia watu wake zaidi ya mara 3000 kwenye kipindi cha zaidi ya miaka 70. Hakuna kiongozi mwingine mwenye uzoefu mkubwa kiasi hiki lakini pia hakuna mtu aliyejisemea kidogo kuhusu maisha yake kama kiongozi na uzoefu wake kama Malkia Elizabeth II. Malkia Elizabeth II hakuwahi kuingilia masuala ya kisiasa hadharani, hakuwa akifanya mahojiano, alikuwa msikivu zaidi kuliko kuongea, hakupenda mafarakano na alikuwa akijitoa. Hii ndio sababu kuu watu wengi walimpenda sana. Hata hivyo, kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho. Malkia pamoja na viongozi wake walifahamu hili na hivyo waliamua siku nyingi kuweka mipango ya awali ya matukio yatakayokuja baada ya kifo chake, mipango ambayo iliidhinishwa na Malkia mwenyewe (licha ya kuwa idhini ya mwisho itatoka kwa Mtawala atakayefuata). Kumeshakaliwa vikao mbalimbali kati ya taasisi nyingi zinazohusika moja kwa moja, serikali ngazi za chini n ahata ngazi ya taifa, ngazi mbalimbali za jeshi la uingereza, mamlaka za kidini na wawakilishi mbalimbali kutoka nchi zote kumi na tano alizokuwa akitawala Malkia.
Prince Charles moja kwa moja anakuwa Mfalme kufuatia kifo cha mama yake. Yeye ataitwa King Charles III na ataongoza si tu Uingereza, bali nchi zingine 14 ikiemo Australia na Canada na pia ataiongoza Jumuiya ya Madola.
Kwa ujumla, swali moja lilosalia kuhusu Malkia Elizabeth II ni kama angeweza kudumu madarakani kwa muda wote huo kama naye pia angejihusisha moja kwa moja na kuingilia mambo ya kisiasa. Wafalme waliomtangulia waliishia kumaliza tawala zao kutokana na maamuzi ya pupa hasa kwenye utungaji wa sera na maamuzi ya kisiasa waliyoyafanya. Mafunzo mbalimbali ya kihistoria yamehusisha uvuguvugu (neutrality) wa Malkia Elizabeth II na umaarufu wake kwa jamii ya wengi. Pengine somo la kujifunza hap ani lile lile; yaani huu ni mvinyo ule ule wa zamani lakini kwenye chupa mpya tu. Kwamba ni heri kujifunza kunyamaza na kufanya kilicho sahihi.
Mungu akubariki kwa uandishi mzuri. nimefurahii uandishi wako.
ReplyDelete