BIASHARA YA VIDOLE VYA MIGUU NCHINI ZIMBABWE: Ni nini hasa kinaendelea?
“Nchini Zimbabwe, watu wameanza kuuza vidole vya miguu yao kwa maelfu ya dola. Hii ni kutokana na gharama za juu za kimaisha na serikali kushindwa kutengeneza ajira.” Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa kwenye mtandao wa Twitter siku nne zilizopita kupitia akaunti ya @InnocentZikky, chapisho ambalo pia limeeleza kuwa vidole hivi huuzwa kwa dola kimarekani 20,000 kwa vidole vidogo (sawa na Milioni 46 ya kitanzania) na dola 40,000 kwa vidole gumba (sawa na Milioni 93 za kitanzania). Chapisho hili liliambatanisha maneno hayo pamoja na picha ya mguu usio na vidole vyote, picha mojawapo kati ya picha tatu. BBC imeripoti kuwa mwanablogu mmoja wa Zimbabwe amedai biashara hiyo inafanyika katika kituo kimoja cha maduka katika mji mkuu wa Harare. Tetesi zaidi zinasema kuwa vidole hivi hutumiwa na watabibu wa kitamaduni wakijulikana kama waganga bandia wanaohusishwa na imani za kishirikina. Waganga hawa hushutumiwa na waganga wa kienyeji wanaotambulika kwa jina la ‘sangoma’ katika baadhi ya maeneo kusini mwa bara la Afrika.
Hadi sasa kufikia kusambaa katika nchi mbalimbali kama Tanzania na Nigeria, nchini Zimbabwe taarifa hizi zilisambaa mtandaoni huku watu wengi wakiambatanisha picha na ‘hashtag’ #Chigunwe ikimaanisha vidole vya miguu kwa watu wa Shona. Hata hivyo, gazeti la burudani la H-METRO nchini humo limeripoti kuwa serikali ya Zimbabwe imekanusha taarifa hizo zinazosambaa mtandaoni ambazo mwanablogu kwa jina la Gambakwe alichapisha mnamo tarehe 28 mwezi Mei kwamba biashara ya kuuza vidole inaendelea katika duka kuu la Ximex Mall na kwamba wanaofanya biashara hiyo wananunua vidole vya miguu kwa pesa nyingi. Wafanyabisahara katika maduka hayo wamekanusha taarifa hizi huku mfanyabiashara mmoja ambaye mwanzo alidai kuwa kuna ukweli katika taarifa hizi naye pia alikuja kukanusha akidai alikuwa amelewa na alikuwa anatania tu. Serikali nchini humo pia imetoa onyo kali kuwa wanaosambaza taarifa hizo potoshi na za uongo mtandaoni huku ikisisitiza kuwa wanajiweka katika hatari ya kukamatwa.
Akizungumza na shirika la Habari nchini Zimbabwe, ZBC, Naibu Waziri wa Habari na Utangazaji, Kindness Paradza alisema serikali imelifanyia uchunguzi suala hilo na kugundua hakuna ukweli wowote kuhusiana na sakata hilo. Aliongeza pia kuwa, watu wanaosambaza taarifa hizi wanadhamiria kuharibu taswira ya wananchi wa nchi hiyo wanaofanya kazi kwa bidii kujikimu kimaisha kwa kuleta dhahania ya kuwa wanauza vidole vyao ili kujipatia kipato.
Wafanyabiashara wa Ximex Mall wamepanga siku ya kesho kwenda kazini wakiwa wamevalia mavazi maalumu (‘slops’ katika lugha ya kiingereza) kuionyesha dunia kuwa vidole vyao vyote vipo salama kabisa.
Aiseee! kumbe Sio kweli Ni taarifa za uzushi tu,
ReplyDelete